breaking news

YANGA WANAPO NIKUMBUSHA ULE MSEMO WA KISWAHILI TENDA MEMA NENDA ZAKO.

February 22nd, 2017 | by mwana kabumbu
YANGA WANAPO NIKUMBUSHA ULE MSEMO WA KISWAHILI TENDA MEMA NENDA ZAKO.
Fikra
0

Na Aidan Mlimila

Wakati nikifuatilia mechi ya fainali ya kombe la Mataifa ya Afrika mapema mwaka huu kati ya timu ya Taifa ya Cameroon dhidi ya Timu ya Taifa ya Misri, mechi iliyoisha kwa Cameroon kutwaa kombe hilo kwenye fainali zilifanyikia nchini Gabon. Kuna vitu viwili vilinivutia kutoka kwenye mchezo ule, kitu cha kwanza ni lile goli maridhawa lililofungwa na Vicent Aboubakar  ambalo liliwahakikishia Cameroon ( Indomitable Lions) kombe lao la tano la AFCON ambalo walilisubiri  kwa siyo chini ya miaka 15 tangu wafanye hivyo mara ya mwisho mwaka 2002.

Kitu cha pili ambacho kilinivutia zaidi ni kile ambacho nilikiona kutoka kwa wachezaji wa Cameroon mara baada ya mechi kuisha. Waliingia ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo na wote kwa pamoja wakatoka wakiwa wamevaa T-shirts zenye namba 17 mgongoni. Ilikuwa ni namba 17 ambayo kwanza kabisa ilikuwa inahashiria mwaka ambao wametwaa ubingwa lakini kikubwa zaidi ilikuwa inahashiria  kumuenzi mmoja kati ya watu ambao walijitoa kwa kiasi kikubwa sana akiwa na jezi ya timu ya Taifa ya Cameroon na huyu si mwingine ni marehemu Marc Vivien Foe.

Ikumbukwe kuwa Marc vivien Foe alifariki mwaka 2003 akiwa analitumikia Taifa lake kwenye michuano ya kombe la mabara nchini Ufaransa. Mbali na kuwa ilikuwa imeshapita takribani miaka 14 tangu Foe alipofariki lakini bado Cameroon wameendelea kumuenzi na kuthamini mchango ambao Foe alikuwa anautoa kwa Taifa lake enzi za uhai wake.

Ni takribani wiki mbili au tatu zilizopita nilipata taarifa za kuugua kwa mmoja kati ya viungo bora nchini Tanzania kwa  miaka ya karibuni marehemu Geofrey Bonny. Kuna vitu viwili vikubwa vimenisikitisha sana kwenye hili la Marehemu Bonny (Ndanje) kwanza kabisa ni namna ambavyo marehemu Bonny alivyopata matibabu yake kwa shida. Kwa hadhi ambayo Bonny alikuwa nayo ilikuwa ni kitu cha kusikitisha sana hasa ukizingatia ni ukweli usiopingika kuwa Geofrey Bonny alicheza  kwenye levo ya juu kabisa ya mpira wetu akiwa na Yanga pamoja na timu ya Taifa.

Ni vizuri kwa wachezaji hawa wanaocheza kipindi hiki kujaribu kuwekeza kwa maisha yao ya baadae kwa kujiunga na mifuko mbali mbali ya bima ambayo itawasidia kwenye mambo ya matibabu pale ambapo mfumo wetu mbovu wa soka utakapo kuwa umewatema. Lakini kitu kikubwa zaidi ambacho kimenisikitisha zaidi na kufanya nikumbuke kile ambacho wachezaji wa timu ya taifa ya Cameroon walikifanya usiku ule pale stade de lA’mitie jijini Libraville nchini Gabon mara baada ya mechi ile ya fainali kuisha ni namna ambavyo Geofrey Bonny alivyoshindwa kupewa heshima ambayo kimsingi alistahili kupewa kwa kuthamini mchango mkubwa aliowahi kuutoa akiwa na jezi ya timu ya taifa na klabu yake kipenzi ya Yanga.

Ilikuwa ni jumamosi ya tarehe 18, siku ambayo klabu ya Yanga ilikuwa inacheza mchezo wa marudiano dhidi ya timu ya Ngara Fc kutoka Comoro na siku hiyo hiyo pia ilikuwa ni siku ambayo mwili wa marehemu Bonny ulikuwa unaenda kupumzisha kwenye nyumba yake ya milele jijini Mbeya ambako ni nyumbani kwake (coincidence). Kwa hali ya kawaida nilitegemea kuona klabu ya Yanga ambapo ndiyo mahali ulimwengu wa soka ulipoanza kmfahamu sawa sawa ikijaribu kumuenzi na kuoneshwa kuguswa siku ya mchezo wao na Ngaya ambayo pia ilikuwa ni siku ya mazishi.

Lakini cha kusikitisha na kwa mshangao wa wengi hakukuwa na tukio lolote lile ambalo lilifanywa na klabu ya Yanga kuonesha kuguswa kwao na msiba wa mmoja kati ya watu ambao walitoa mchango mkubwa sana akiwa na jezi ya klabu ya Yanga enzi za uhai wake. Achana na yanga kuvaa T-shirt ambazo zingemuenzi Bonny kama kile ambacho wachezaji wa Cameroon walikifanya pale Gabon basi nilitegemea kuona walahu Yanga wangeweza kusimama hata kwa dakika moja kabla ya mchezo kuanza na kumuenzi kwa kumuombea dua fupi lakini hata hilo pia lilionekana kuwa ngumu kwao.

Ni jambo la kusikitisha na kukatisha tamaa hasa hasa kwa hawa wachezaji ambao wanavitumikia hivi vilabu kwa wakati huu. Mtu mwingine anaweza akahoji ulazima wa Yanga kufanya hiki ambacho wadau wengi wanajaribu kuhoji lakini ukweli ni kwamba siyo lazima kufanya hiki ambacho watu wengi tunadhani Yanga walipaswa kufanya lakini ni jambo nzuri kibinadamu kuenzi na kuthamini mchango wa mtu ambaye ametangulia mbele za haki. Na hapa ndipo ninapo kumbuka ule msemo wa kuwa kuna mpira wa Tanzania na kisha kuna mpira wa Duniani, na kabla sijamaliza kutafakari nakumbuka ule msemo wa Kiswahili tenda mema nenda zako.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *