breaking news

SERIKALI KUTENGA SHULE MAALUM KWA AJILI YA MICHEZO

January 30th, 2017 | by mwana kabumbu
SERIKALI KUTENGA SHULE MAALUM KWA AJILI YA MICHEZO
Kitaifa
0
Na: Imani Kelvin Mbaga, Dar es salaam.
Serikali imeamua kuanza kuwekeza katika michezo kwa kutenga shule 55 za sekondari ambazo zitakuwa za mchepuo wa michezo na kuchukua wanafunzi watakao fanya vema katika masomo na michezo ili kuinua michezo nchini na kuiletea sifa Tanzania pamoja na kutoa ajira kwa vijana.
Hayo yamesemwa leo na mkurugenzi wa michezo nchini, Omar Yusuph Sinde wakati akizindua mpango maalum wa kuandaa vijana wadogo watakaoshiriki michuano ya Olimpiki inayotarajiwa kufanyika huko Tokyo nchini Japan mwaka 2020.
Sinde alisema kuwa kutokana na ukweli kwamba hakuna maendeleo katika mchezo wowote yanayoweza kufikiwa isipokuwa kwa kuwaandaa vijana wadogo ambao wakiandaliwa vema wanaweza kufanya vizuri na kuitoa nchi kimasomaso katika sekta ya michezo.
“Tunafahamu kuwa wadau wa michezo wamekuwa wakidai mara kwa mara suala la kuwaandaa vijana wadogo, na serikali imeliona hilo ndo maana zinaandaliwa shule 55 za sekondari ili zitumike kuwaandaa vijana” Alisema Sinde
“Hata leo tunapoongea haya kuna kikao kinachoendelea mjini Dodoma cha watendaji katika wizara tano tofauti kujadili juu ya suala hili, kwakuwa ni suala mtambuka, lakini tuko makini katika hili” Aliongeza mkurugenzi huyo
Aidha Sinde alisema kuwa wanafunzi watakaochukuliwa ni wale watakofanya vizuri katika michezo ya shule za msingi yaani UMITASHUMTA, na kwamba wale watakaofanya vizuri katika masomo na michezo ndiyo watakaopata nafasi ya kusoma katika shule hizo
Wakati huohuo, serikali imelipongeza shirikisho la soka nchini kwa kuandaa mpango wa kuwaendeleza vijana na kuahidi kuwa nalo bega kwa bega katika kuhakikisha kuwa mipango hiyo inatekelezeka kwa wakti kwakuwa Watanzania wamechoka kuwa wasindikizaji katika michuano ya kimataifa.
Uzinduzi huo ulifanyika katika viwanja vya Karume jijini Dar es salaam na kuhusisha wadau mabalimbali wa soka nchini wakiwemo wale wanao shughulikia soka la vijana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *