breaking news

MKWASA AREJEA YANGA, SASA NI KAMA KATIBU MKUU

February 1st, 2017 | by mwana kabumbu
MKWASA AREJEA YANGA, SASA NI KAMA KATIBU MKUU
Kitaifa
0
Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya kandanda Tanzania bara, klabu ya Yanga ya jijini Dar es salaam, imemteua nahondha na kocha wake wa zamani, Charles Boniface Mkwasa maarufu kama “Master” kuwa katibu mkuu mpya wa klabu hiyo kwa muda wa miaka miwili.
Akitangaza uteuzi huo mbele ya waandishi wa habari, katika makao makuu ya klabu jijini Dar es salaam, makamu mwenyekiti wake, Clement Sanga alisema baada ya uongozi kutafakari kwa kina wameona kuwa Mkwasa ni mtu sahihi wa kuifanya kazi hiyo.
“Mkwasa ni mchezaji wetu wa zamani na uzoefu wa soka la Tanzania kwa kuwa amelitumikia katika ngazi za juu, naamini uzoefu wake utatusaidia kuipeleka klabu mbele” Alisema Sanga
Sanga pia alisema hii inaweza ikawa njia mojawapo ya kuwafanya wachezaji wa zamani, walioutumikia mpira wa nchi hii kujiona kuwa ni sehemu ya familia ya soka la Tanzania, na kwamba huo unaweza kuwa mwanzo wa Mkwasa na wengine kuingia katika kada ya uongozi.
Naye kocha huyo wa zamani alisema anaushukuru uongozi kwa kumpa nafasi nyingine ya kuitumikia klabu hiyo, na akaahidi kuifanya kazi yake mpya kwa uaminifu, huku akiwaomba mashabiki na wanachama kuwa watulivu na kushikamana ili waweze kufanya vizuri.
Mkwasa ameitumikia klabu hiyo kwa nafasi tofauti, akiwa kama mchezaji, nahodha na kwa nyakati tofauti amekuwa kocha msaidizi na kocha mkuu, hivyo ni miongoni mwa wanachama wanaoufahamu vema utamaduni wa klabu hiyo.
Wakati huo huo makamu mwenyekiti huyo amtolea ufafanuzi juu ya klabu yake kukataa kucheza mechi ya kirafiki na mabingwa wa Afrika kwa upande wa vilabu, timu ya Mamelodi Sundown kutoka nchini Afrika ya kusini, ambao wapo nchini kupiga kambi ya siku nne.
Sanga alisema kuwa benchi lao la ufundi ndilo lililokataa kucheza mechi hiyo, kwa sababu ya mazingira na ratiba ya ligi inayoendelea, kwakuwa wanakabiliwa na kibarua cha kuutetea ubingwa wao, kwa mechi zilizopo mbele, ambapo watacheza na Stand united katika mchezo unaofuata.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *