breaking news

KUNA WAKATI HAUHITAJI PESA KUPATA KILICHO BORA MAISHANI..

May 11th, 2016 | by mwana kabumbu
KUNA WAKATI HAUHITAJI PESA KUPATA KILICHO BORA MAISHANI..
Fikra
0

FIKRA ZA MWANAKABUMBU

Na Aidan Mlimila

Kuna kipindi rais wa kwanza wa Afrika ya Kusini, Hayati Nelson Mandela aliwahi kunukuliwa akisema “Pesa haiwezi kuleta mafanikio bali uhuru wa kujiamulia ndiyo unaoweza kuleta mafanikio”.

Ni ngumu sana kwa dunia ya sasa kuamini kile ambacho Hayati Nelson Mandela alikiamini, hasa kwa kipindi hiki ambacho chochote unachofanya unahitaji pesa ili kuweza kukifanikisha. Ni katika kipindi hiki hiki ambapo mwenye msuli wa pesa ndiye anaweza kuishi na kufanikisha lolote analolifanya huku yule ambaye hana msuli mkubwa wa pesa akikutana na changamoto katika kile ambacho anahitaji kukifanikisha.

Katika zama hizi za mpira wa kisasa (Modern Football) inaaminika ili uweze kushindana na kupata mafanikio ya ndani ya uwanja basi ni lazima uwe na msuli mkubwa wa kifedha. Ni lazima uwe na uwezo wa kuingia sokoni na kushindana kupata wachezaji bora ambao watakuwezesha kushinda mataji.

01C5982600000514-3340701-image-a-40_1448958869085

Ni katika zama hizi za mpira wa kisasa tumeshuhudia pia pesa za mafuta kutoka kwa waarabu zikizidi kutuaminisha kuwa pesa ndiyo kila kitu katika mafanikio ya mpira wa kisasa. Tumeshuhudia wawekezaji wengi kutoka Uarabuni wakijaribu kufanya uwekezaji wa pesa zao za mafuta katika vilabu mbali mbali barani Ulaya. Ni ngumu kuipinga nguvu ya pesa katika zama hizi za mpira wa kisasa.

Kabla ya Agosti mwaka jana (mwezi ambao msimu wa ligi kuu Uingereza huwa unaanza) ilikuwa ni rahisi kuamini kuwa Edward Lowassa ndiye raisi ajaye wa awamu ya tano, ilikuwa ni rahisi kuamini Kiiza Besigye ndiye raisi ajaye wa Uganda. Kabla ya Agosti mwaka jana ilikuwa ni rahisi kuamini kama Jose Mourinho na kikosi chake wangeweza kutetea ubingwa wao msimu huu, ilikuwa ni rahisi kuamini kuwa Man Utd ya Van Gaal ingeweza kuwa mabingwa wa Epl msimu huu.

Bado ilikuwa ni rahisi tu kuitabiria Arsenal ya Alexis Sanchez au Man City ya Yaya Toure kuwa ndiyo mabingwa wa Epl msimu. Unajua kwanini? Hauhitaji nguvu nyingi sana kujua ni kwa nini, jibu ni rahisi sana unapozungumzia timu ambazo zinaonekana kuwa na nguvu kubwa kiuchumi au timu ambazo zinaundwa na wachezaji wengi ambao dunia inawatazama kama ni wa viwango vya dunia katika ligi kuu ya Uingereza basi hautaacha kuzitaja Man City, Arsenal, Man Utd na Chelsea pia.

Ilikuwa ni ngumu sana kuamini kama Leicester City ya Danny Drinkwater kuwa bingwa wa ligi kuu ya Uingereza msimu huu au Spurs ya Delle Ali kumaliza ndani ya timu tatu za juu. Falsafa ya mpira wa kisasa ambayo siku zote huwa inaamini katika matumizi ya pesa ndiyo iliyotufanya tusiamini kuwa Leicester City ingeweza kumaliza walau ndani ya timu nne za juu.

danny-drinkwater-1170x658

Claudio Ranieri amejaribu kutuaminisha kuwa kumbe unaweza kwenda kusikojulikana ukamchukua Ng’olo Kante, unaweza ukaenda kusikojulikana ukamchukua Jamie Vardy, ukaenda kusikojulikana ukamchukua Riyard Mahrez, ukaenda Stoke City ukamchukua mjerumani mwenye roho ngumu Robert Huth, ukaenda pia jijini Birmingham ukachukua zao la Academy ya Aston Villa Mark Albrighton ukaja ukawaweka pamoja na kutengeneza timu bora na kufanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi maarufu duniani.

Ingawa bado watu wengi wanaamini kuwa mafanikio ya Leicester City msimu huu yametokana na kufanya vibaya na kukosa muendelezo wa matokeo kwa timu kubwa lakini binafsi sidhani kama unahitaji elimu ya form six kuamini Leicester City msimu huu walikuwa na timu bora pasipo kuingia sokoni na kutumia pesa kupata wachezaji wenye majina.

Katika zama hizi ambapo pesa za mafuta kutoka uarabuni zimeutawala mchezo wa soka hasa barani Ulaya ni nadra kwa timu ambayo haina mfuko uliotuna kuweza kufanya hiki ambacho Muitaliano Claudio Ranieri amekifanya msimu huu akiwa na timu ambayo msimu uliopita ilipambana kutoshuka daraja tena katika ligi ambayo Sheikh Mansour ameweka pesa zake za mafuta.

Nguvu ya pesa ndiyo iliyotufanya tuamini kuwa ni haki kwa Man City, United au Chelsea kuvaa medali za ubingwa wa ligi kuu ya Uingereza huku tukiamini kuwa ni mwiko kwa Leicester City, au Spurs ya Pochettino kuwa ndani ya timu mbili au tatu za juu katika msimamo wa ligi. Claudio Ranieri amefanikiwa mtihani wa kwanza wa kuishinda nguvu ya pesa kwa kutengeneza timu bora pasipo kutumia pesa nyingi lakini wasiwasi mkubwa ni kama atafanikiwa kuushinda mtihani wa pili na huu si mwingine bali ni kuhakikisha anawilinda wachezaji wake wengi muhimu kutomezwa na timu ambazo zina msuli mkubwa kipesa.

Leicester_3_croppe_2844470b

Bila shaka huu ni mtihani mgumu sana kwa Claudio Ranieri na ndiyo hapa ambapo nguvu ya pesa itadhihirika ni ngumu kumzuia Ng’olo Kante kuondoka msimu ujao, ni ngumu kumzuia Riyad Mahrez kwa uwezo waliounyesha msimu huu. Na ngumu kwa sababu klabu kama Leicester City inahitaji pesa kuweza kujiendesha na mauzo ya wachezaji ni moja kati ya vyanzo vikubwa vya mapato kwa timu kuweza kujiendesha.

Bado ni ngumu kuikataa paundi milioni 20 kwa timu kama Leicester City ambayo kuichumi haiko sawa. Claudio Ranieri ametengeneza kilicho bora pasipo kutumia pesa nyingi lakini itakuwa ngumu kwake kuweza kuilinda bidhaa hii bora kabisa ambayo ameitengeneza msimu huu. Bidhaa ambayo kwa siku za karibuni imekuwa maarufu pengine kuliko mwanamuziki Beyonce.

3381D87000000578-3556666-image-m-2_1461533364993

Alichokifanya Claudio Ranieri ni kitu kidogo tu, nacho si kingine bali ni kutofuata na kuziamini falsafa za mpira wa kisasa na kuishi katika falsafa nyingine ambayo ni “Hauhitaji pesa kupata kilicho bora Maishani”.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *